Social Icons

Wednesday 5 February 2014

NI MUHIMU WAZEE WATAALAM AMBAO WAMESTAAFU WATUMIKE KUJENGA TAIFA.



Ndugu mdau,
Habari yako, leo nakuja na mada hii ya wataalamu wa fani mbalimbali ambao wamestaafu muda mrefu.
Tanzania imebahatika kuwa na wataalamu wengi ambao wamepita katika Nyanja nyingi katika ajira serikalini hata katika mashirika, taasisi, wakala mbalimbali.  Wapo ambao walikuwa wanaaminika sana kwa uchapaji wao wa kazi, mawazo yao, muda mrefu wa kufanya kazi, uelewa na utambuzi wao ulioifanya Tanzania kuwa juu katika nyanja mbali mbali.
USHAURI WANGU
Haiwezekani kuanzishwa taasisi fulani ambayo itakuwa imesheheni wataalamu hao na kuwapa heshima ya kuwa wanafanya kazi kwa mkataba ili kuwapa motisha ili wasiumie katika kufuatilia mafao yao na pia utaalamu walio nao usife kabisa?  Na wale wengine basi hata wakianzisha miradi yao ya ukulima au ufugaji au hata ujenzi wa nyumba zao za kupangisha basi wapewe heshima ya miradi yao ili waweze kujipatia kipato!
Ninawaona wazee wengi wakiwa wamevaa ndala ndefu zilizowazidi miguuni mwao, wakiwa na nywele nyeupe tii, suruali zao zikiwa zimefungwa mkwiji, huku wakiwa wameshika magazeti ya zamani wakitembea huku na kule wakiwa hoi kwa njaa, na mawazo na uwezo wao wa kichwani ukiwa unatafunwa na uzee na mihangaiko wanayopata masikini, huku tukiwaangalia na kuwadharau hata wakiingia katika madaladala kwa kutowapisha katika viti, kisa hatuwajui na wamefanya makubwa sana katika nchi hii, iwe serikalini, michezoni, jeshini na sehemu nyingine.
Wengine hata wanapofuatilia mafao yao huambiwa walete CV, Barua ya ajira hivi kweli mtu alianza kazi mwaka 1970 huko leo atakuwanayo, sawa anaweza kuwa navyo vinafanyiwa kazi kwa muda? Kiinua mgongo anachopata cha miaka ya kale hakiendani hata na wakati huu kweli si tunatengeneza laana tu?
Kwanini tunawasahau wazee hawa wanakufa kihoro, wanakufa huku wakilalamika, wakisikitika, wengine wakiishi huku wakiwa wamekata tamaa  kabisa na kutoa laana kwa serikali.  Naumia sana kuona wazee hawa wakiwa hawana la kufanya zaidi ya kuwa kama wamachanganyikiwa.
Hivi hatuoni kuwa tunatengeneza nchi ya kuwahi chako haraka ili ukifikia uzee usiwe kama hawa tunaowaona kwa sasa?  Nawaomba sana jamani ambao mna shikilia sehemu ambazo zinaweza kwenda kujifunza mambo nje basi mkajifunze nchi za wenzetu wale wazee wakistaafu huwa wanatumikaje katika kuleta manufaa kwa nchi na sikuwa sahau hivi jamani.
Kwa kweli inauma sana, unakuta mtu hata ana sehemu yake ya ardhi hata iwe hekari 100, lakini anafuatilia hati miaka 30 haipati, mwisho anaonekana amehodhi ardhi bila kuitumia inavyotakiwa, mwisho linakuja wazo la kitoto kabisa eti aiachie serikali igawe kwa wengine huu ni unyama wa hali ya juu, tunatengeneza laana mbaya sana aisee, siafiki hiki kitu, na watanzania tulio wengi tunashangilia kabisa wakati yule mtu ametumikia nchi kwa miaka zaidi ya 30, na ile ndio kiinua mgongo chake, pale ndio anategemea hata awaachie wanae, ninyi hamumthamini kabisa wala kwanza hamtaki hata kuelewa, mimi nasema ni dhambi na dhambi hii itakuja kutuunguza hapa hapa duniani.
Hebu tujaribu kuvaa yale maumivu yao, machungu yao, utendaji kazi wao walioutenda kwa kujituma na uaminifu kwa miaka mingi iliyopita halafu mwisho wananyanyasika.  Inauma sana jamani.
Ndio  unatakiwa kujiandaa ili ustaafu, mzee wa watu ndio kajiandaa kanunua ardhi yake ili aje alime sasa unapomzungusha miaka nenda rudi unamaanisha unataka afe ili iweje?
Mfano mtu anastaafu na miaka 55 hadi 65 labda unamzungusha miaka 25 hadi 30 kufuatilia hati atakuwa na miaka mingapi hapo?
Najaribu tu kukumbusha wahusika, na sisi wananchi tujaribu kuliona hili lina tija.

HITIMISHO
Tujali maisha ya wengine
Tutumie wataalamu waliomaliza muda wao wa kazi na walifanya kazi kwa ueledi na kuwapa heshima kwa kuwapa taasisi moja yenye vipaji vyote humo.
Hii itachangia kuwapa motisha hata hawa waliopo madarakani wasiwaze kujilimbikizia mali pasipo sababu kwa kuwa nao wanasoma maisha ya waliopita.

No comments:

Post a Comment

Asante kwa ku Comment yako ujumbe wako ni muhimu