Social Icons

Featured Posts

Tuesday, 11 February 2014

SOMO LA LEO: JIFUNZE JUU YA AJALI ZA MOTO,KUJIKINGA NA KUTUMIA VIFAA VYAKE



AJALI YA MOTO NA VITENDEA KAZI VYAKE

Ni kitu gani husababisha moto?
Swali hili ukimuuliza mtu yeyote asiye na ufahamu na moto hatakuwa na jibu sahihi.
Chanzo cha Moto ni moto wenyewe, hili ndio jibu halisi.
Kuna aina nyingi za moto;
1.      Moto wa Umeme
2.      Moto wa Mlipuko
3.      Moto wa kuanzishwa na Mtu
4.      Moto Unaozuka Wenyewe kutokana na mlundikano wa vitu, kama majani na vitu vingine
5.      Na Kadhalika

Wengi wetu hatufuatilii kuhusu elimu hii ya moto tukiamini wapo wanaozima moto, lakini naomba nikuambie mdau wa blog hii, hakuna kazi ya mtu mmoja katika majanga hasa ya moto.  Huwa tunawalaumu sana Kikosi cha Zimamoto kwa kuwa huwa hatujui ni adha gani wanaipata, ingawa mimi nawalaumu kwa upande mwingine kuwa ilibidi hata wangekuwa wanakwenda kama wanasiasa katika majukwaa kwa kutoa matangazo kuwa siku Fulani tarehe Fulani, saa Fulani tutakuwa sehemu Fulani tutatoa elimu kuhusu majanga ya moto.  Hii yote ni kujaribu kutapakaza elimu hii adimu ya kujiokoa na kuokoa katika ajali za moto wa aina yoyote.  Heri wananchi wengi wapate kitu kidogo watakacho ambulia kuliko walivyo sasa hawana uelewa wa kitu chochote kile.
Je ni mwananchi gani wa kawaida anajua jinsi ya kutumia fire extinguisher, ni aina gani ya fire extinguisher itatumika katika moto wa uliosababishwa na shoti ya umeme, na ni fire extinguisher gani itatumika katika moto uliosababishwa na mafuta, ni fire extinguisher gani itatumika ikiwa moto umesababishwa na moto kutoka jiko la mkaa ukarukia nguo, ukaenda katika godoro au makuti na kuwaka.
Je ikiwa mtu katika ajali ya moto, nguo zake zimeshika moto labda mgongoni atatakiwa kufanya nini kabla ya yote, je mtu akiona moto unawake tangu awali anatakiwa kufanya nini kabla ya kupiga simu kituo cha zimamoto na kutoa taarifa zilizo sahihi ili zimamoto waje na gari husika kwa moto husika.  Maana sio kila gari ya zima moto inazima moto wowote.
Je wakati unapambana na moto unajilindaje na moto unaopambana nao?  Amini usiamini moto una akili sana, na ndio maana tunasema kupambana na moto sio kuzima moto, moto unauwezo wa kukuchungulia na kukusoma ulivyo kwa wakati huo na kukushambulia kama hujui, moto una shambulia kwa malengo, kama hutakuwa makini moto unakuua mara moja.  Ni haki yako mtanzania kujua jinsi ya kupambana na moto mdogo hadi mkubwa, wa majumbani hadi misituni.  Tambua vifaa vyote au vichache vya kuzuia na kuzima moto.  Ni hatari sana utakuta tunaishi katika majumba hatuna hata sehemu za kukimbilia kama kutatokea tatizo la moto, nyumba hazijakaa kitaalamu sana, likitokea la kutokea na grills tunazoweka siku hizi hatoki mtu ndani.  Nyumba tunajenga bila malengo, hakuna anayewaza janga la moto.  Ndio moto hutokea mara moja kwa miaka kadhaa ila hiyo siku moja inakurudisha sifuri kabisa kama hukuwa na kitu.  Ni wangapi tuna bima za nyumba labda, ni wangapi tuna bima za maisha, zaidi ya bima ya gari tena kwa kuwa utakamatwa na trafiki barabarani, na bima yenyewe tunakata third party mnaita.  Kama nilivyosema blog hii itakuwa inakukumbusha au kukupa kitu kipya ambacho unakijua lakini hukifuatilii na huna hata wazo nacho, lakini kikitokea ni lawama lawama kwa kila mmoja kuona anaongea sahihi kumbe tatizo tunalo katika jamii huku.
Leo mimi nitakufundisha kidogo sana kuhusu kuzima moto kwa kutumia ile mitungi ya kuzimia moto fire extinguishers’

Wenyewe fire au zimamoto wana maneno yao wanaita PASS
P = PULL (ONDOA PIN)
A = AIM (ELEKEZEA MPIRA WA KUZIMIA KATIKA MOTO SIO KATI MWANZO)
S = SQUEEZE (BINYA ULE MKONO WA KURUHUSU MAJI AU UNGA KUTOKA)
S = SWEEP (PELEKA MKONO WAKO WA KUSHOTO KULIA NA KUSHOTO)

Mtungi ule hushikwa na mkono wa kulia, na ule mpira wa kuzimia hushikwa na mkono wa kushoto, wanaposema toa pin sio pin number, kuna pin utaona imewekwa kwaajili ya kuzuia maji au unga uliomo ndani ya mtungi yasitoke au usitoke.  Angalia mazingira ya moto ulipoanzia halafu elekezea ule mpira wa mtungi sio katikati ya moto, utaungua na hutakuwa unafanya kitu, anza kupambana nao kama unaanza kula sambusa hivi, pembeni pembeni hadi unajua chanzo, pia soma upepo unakotoka na kuelekea, kwa kuwa ukipingana na upepo utacheza pata potea.  Moto huwa unakaa upande ambao wewe ni kikwazo kwako, wakati wewe unatafuta hewa wenyewe unaichukua ile hewa na kukupa wewe wakati mgumu.  Ukishajiweka katika mazingira mazuri ya kutambua hayo yote basi pambana nao.
Na kama ni ndani ya jingo kumetokea moto na ni lazima ufungue mlango ili utoke ndani ya korido, unashauriwa usifungue kwanza mlango hadi uhakikishe kuwa moto haujafika mlangoni, kwa sasa majengo mengi ya mjini ni magorofa, yana miundo tofauti na nyumbani, ikiwa unataka kutoka kwanza gusa mlango kama unaupima joto, kwa style ya kama unampiga mtu kibao cha kerebu, maana huko ndio kuna hisia nzuri za kitu, ukihisi joto sana usifungue maana utakutana na moto ambao utakuua,na utasababisha oxygen kuingia kwa wingi katika chumba hivyo utauita moto kwa nguvu sana.
Hakikisha unafuata taratibu zote bila ya kupiga kelele au kuchanganyikiwa kwa kuwa unapofanya hayo utapoteza nguvu na utabaki katika moto, tafuta EXIT sehemu za kutokea ili ujikwamue. 
Ikiwa bahati mbaya moto umekushika mgongoni lala chini haraka, kisha jigeuzegeuze ili uuzime, usikimbie huku unapiga kelele utakuwa unazidi kuuchochea na utaungua vibaya.
Nakuomba kuanzia leo hakikisha popote unapokaa pawe na njia ya kukimbilia ikiwa itatokea janga la moto.  Epuka kujaza maganda ya Apples (Tufaa) sehemu moja, au makaratasi mengi au majani mengi sehemu moja kwa muda mwingi hivi husababisha moto bila kiberiti, ndio maana unaweza shangaa msituni moto unaanza tu bila mtu kuuwasha, na wengi wetu huhisi mtu katupa kichungi cha sigara, si kweli kwa asilimia kubwa, majani nayo ni chanzo kizuri cha moto.
Kuna vitendea vingi vya kuzuia na kuzima moto;
1.      Mitungi ya kuzima moto (Fire Extinguisher)
2.      Magari ya kuzima moto
3.      Ndege za kuzima moto
4.      Meli za kuzima moto
5.      Treni za kuzima moto
6.      Ndoo zenye mchanga wa kuzima moto
7.      NK
Ukiingia katika mitaa yetu hutaona hata sehemu moja yenye bomba la maji ya kuzima moto Hydrants kitu ambacho ni hatari sana, na ndio maana hata wale zimamoto wakifika eneo la tukio wakaanza kupambana na moto maji yaakiisha huondoka na kwenda mbali kujaza maji tena, na foleni na miundo mbinu yetu hii wakirudi wananchi wanakuwa na hasira na kuongea maneno ya hatar hatari wakati hawatambui wale zimamoto ni shida gani wanapata kwa wakati ule.  Inatia huruma sana.
Nakushauri msomaji ukimaliza kusoma hapa ukikutana na mtumishi wa Zimamoto mhoji maswali mawili matatu ili uweze kupata kitu kipya kwake na kitakachokusaidia siku moja.
Unapojenga nyumba jitahidi kuweka eneo maalumu la usalama, pia jitahidi na Inspekta wa zimamoto apitie mchoro wako wa nyumba yako na afike kuhakiki kama umefuata maelekezo katika ujenzi wako.
 
Labda nikuambie au nikupe darasa dogo kuhusu ile mitungi Fire Extinguishers;
KUNA AINA 6 ZA MITUNGI AU TAMBUA MITUNGI HII TOFAUTI YAKE
1.      WATER (UNA KIKARATASI CHEKUNDU [COLOR CODE RED])
2.      WET CHEMICAL (COLOR CODE YELLOW
3.      FOAM (COLOR CODE BLUE)
4.      POWDER (COLOR CODE WHITE)
5.      CARBONDIOXIDE (COLOR CODE BLACK)
6.      POWDER (COLOR CODE YELLOW)
Vile vile hii mitungi imegawanyika katika makundi 6 tena ya matumizi;
Kuna A, B, C, D, E, na F
A.    Wood paper and plastics
B.     Flammable and Combustible Liquids
C.     Flammable Gases
D.    For Fire Including Combustibles metal use special purpose extinguisher
E.     Electrically, Energized Equipments
F.      Cooking Oils and Fats
Hili somo ni kubwa sana linahitaji uelewa na mapenzi ya dhati kabisa kwako.
Okoa maisha yako na ya wengine, kuwa balozi mzuri wa kupambana na majanga ya moto

Swali sasa, kwa mimi, wewe, pamoja na Serikali tumejiandaaje na majanga ya moto kuanzia majumbani, maofisini, vituo vya mafuta, hospitali, shuleni, misikitini, makanisani, viwanjani, katika majumba ya starehe, misituni, maporini na popote pale ambapo janga litatokea.  Jukumu la kutoa elimu hii ni la idara husika ikishirikiana na wizara na serikali kwa ujumla, wananchi tuna haki ya kimsingi kujua jinsi ya kutumia zana hizi, kutambua zana hizi.  Nasi wananchi tukifundishwa tuyashike yale mafunzo ili iwe rahisi kwa lolote litakapotokea.  Kubwa zaidi likitokea janga tusikimbilie kuangalia tutapata madhara makubwa kwa kushangaa kuliko matarajio yetu.

HUU NDIO UVUVI WA KISASA , SOMA HAPA UPATE KUELEWA


Habari ndugu msomaji wa blog hii.

Uvuvi katika nchi yetu hii ya Tanzania unachukuliwa kama utani, unachukuliwa kama mtu akishindwa maisha basi anaingia majini na kwenda kuchukua samaki na kuleta nchi kavu ili wateja tununue.

Uvuvi wa samaki ni kazi tena kazi yenye kipato kikubwa sana katika dunia hii.  Wengi wa wavuvi wetu wanawaza kuchukua mitumbwi na kuanza kupiga makasia kwenda baharini kuvua samaki, lakini sidhani kama kuna wanaokaa na kufikiria kununua meli  kubwa zenye uwezo wa kubeba tani mia mbili na hamsini na kuendelea za samaki kwa siku.  Samaki wenye minofu na wanaotakiwa katika soko ni ni wale walio katika kina kirefu na umbali mrefu ambao boti zetu hizi tunazotumia haziwezi kufika, na hata zikifika huko basi hawawezi kumudu nguvu za maji hayo.

Uvuvi wa kusafiri umbali mrefu na meli kubwa zenye uwezo mkubwa ni njia pekee ya kumnyanyua mvuvi katika uvuvi wake wa samaki, kuna samaki wengi wanaotakiwa katika soko.  Soko ninalo zungumzia hapa ni la ndani na la nje ya nchi.

Ikiwa meli itakuwa na uwezo wa kubeba tani 200 basi kuna uwezekano wa kutengeneza kiasi kikubwa cha fedha kila siku katika uvuvi.  Ikiwa wale samaki walioitwa wa Magufuli walikuwa tani 296.32 wenye thamani ya shilingi bilioni 2.07. ina maana wale samaki walikuwa kila kilo ni shilingi 7,000.
7,000 kwa kilo.  Chukua meli ina tani 296.32, tani moja ni kilo 1,000 x 296,320 = bilioni 2.07 je wale samaki tunaovua pale ferry, na msasani wanafika bei hii kwa siku au wiki? Kama ndio basi wavuvi wamelogwa, kwanini hawaendelei?
Mada hii naiandika nikiwa nawaza kwa uwezo wangu, je kwanini mdau wewe usiidadavue biashara hii ukaona kama inalipa tujiunde kama kikundi kikubwa tununue hata meli moja kubwa (30.2m longline fishing vessel) ambayo ni kama shilingi za kitanzania milioni 500 meli inaweza kuingiza bilioni 2 kwa wiki, hatuoni kuwa tunapoteza muda sana?
Ikiwa wadau 100 tutachanga shilingi 5,000,000 tutapata kiasi cha shilingi 500,000,000 ambacho tunaweza kuagiza meli hii na kufanya taratibu nyingize za kisheria na tukaanza rasmi kazi ambapo meli hii hata kama itaingiza shilingi bilioni 2 kwa mwezi ina maana kwa miezi 12 tutakuwa na shilingi bilioni 24 sasa hapo mdau utakataa kuwa mmoja wa wawekezaji wa meli hii, na hapo tunaweza nunua meli 4 zaidi ambazo zitakuwa zinafanya kazi kwa masoko yote ya samaki.  Samaki watakuwa wakubwa wenye bei rahisi na si visamaki vidogo vya bei ghali tena samaki watazaliana sana kwa kuwa wale wakubwa ndio watakao fuatwa.  Tunaona wavuvi wengi sana wanavamia sehemu za mazalia ya samaki hii inachangia hata kupotea kwa samaki hata katika misimu yao.  Huwezi kupiga vita kuvua samaki kwa net ikiwa wavuvi wana waza leo, kesho Mungu atajua, ni lazima tuwe na mawazo mapana ili tuweze kutokea upande wa pili wa mafanikio.
Serikali inakosa mapato makubwa, wavuvi wanakosa kipato kikubwa, wateja wanakosa samaki wenye ladha na ubora kwa kuwa hakuna vitendea kazi, manahodha wapo wengi meli chache, ikiwa kundi litanunua meli 4 kuna ajira 4 za manahodha, na mabaharia, wavuvi kwa nafasi zao, hapa tutakuwa tumetengeneza ajira pia.  Tutakuwa tumeongeza kipato kwa nchi, kipato kwa familia na kadhalika.


Mdau hebu kaa chini ufikiri halafu utoe mawazo yako hapa.

Monday, 10 February 2014

NI KWELI HAIWEZEKANI KUWA NA SHIRIKA LA NDEGE BINAFSI? SOMA HAPA





SHIRIKA LA NDEGE BINAFSI
Ndugu mdau wa Buberwa Robert Blog,
Najaribu kukupa kitu ambacho nakiwaza kichwani kwangu, kichwa change kimejaa mambo mengi sana ambayo huwa nashindwa kuelewa, je hatuna watu wanao waza, wapo lakini ni mambo magumu, mfumo wetu ni wa kusubiri serikali ifanye nasi tukosoe au kushangilia pale jambo linapoenda kinyume na matarajio ya wananchi?

Leo naomba niongelee kuhusu usafiri wa anga kwa kuanzisha kampuni yetu ya usafiri wa anga itakayoitwa vyovyote wadau watakavyoamua, shirika litakalokuwa na malengo ya kusafirisha abiria ndani ya Tanzania yaani mikoa yote, nje ya Tanzania ikiwa na maana ya Afrika nzima na dunia.  Tutafanyaje hadi tuweze kutokea hadi nje huko duniani, ni mipango ya shirika litaloongozwa na wasomi wenye ueledi wa hali ya juu na si wale ambao kila kitu kwao hakiwezekani.  Ikiwa wenzetu wanaweza kwa nini sisi tushindwe ikiwa tuna saa 24 wote, miaka sawa, tunavuta hewa moja, dunia ni moja ambayo iko katika mfano wa duara, wao dunia yao haipo flat kwanini tushindwe?

Ndugu mdau unayesoma hapa, ninataka utoe mawazo ambayo yatakuwa na tija kwako, kwangu, kwa Yule na wale na Tanzania nzima, leo naongea hili kama ndoto lakini siku likitimia kila mmoja atajisifia, leo hii tunasoma lakini masomo yetu yanatutengeneza tuwe nani, kwanini hatuwi wabunifu, na ubunifu wenyewe uwe wa kuzalisha ajira, kuzalisha fedha, kuzalisha utaalamu na si kusoma na kuzurura na bajasha ukitegemea kuajiriwa, mimi nasema ni aibu kwa msomi mwenye elimu ya juu kutembea na bahasha eti anatafuta ajira, hiyo elimu yako unataka uitumie kwa kufungwa kwa kupangiwa muda wa kazini, mpango kazi usio na tija kwako na familia yako, unawafaidisha waajiri tu ndani ya miaka yote unayofanya kazi.

Leo nakuja na mada ya kufikirika lakini inayowezekana ikitendewa kazi, na si kuidharau na kuona huyu jamaa anawaza nini mbona hiki kitu kigumu, unajua maendeleo yanaletwa na wewe pale unapowaza maendeleo, na si kulalamikia maendeleo yaletwe na mwingine.
Hivi umeshawahi kuwaza kununua ndege labda aina ya Boeing 777 ambayo inauzwa dola za kimarekani 76 milioni, bei ya chini ambapo tunaweza kuwaza kuchanga kwa kiwango chetu na kuchukua mikopo pia ikiwezekana ili tuweze kuanzisha kampuni yenye hata ndege 10 kwanza, ikiwa ndege 2 kubwa za kutoka nje ya nchi jirani, na ndege 8 ndogo za abiria kuanzia 6 hadi 60 zitakazokuwa zinakwenda mikoani kila siku kwa bei nafuu?
 
Wengi wetu tunasomesha watoto, sisi tumeshafubaa, kwanini tusitengeneze kampuni kubwa ya usafirishaji wa anga, kampuni ambayo itaaminika ndani na nje ya nchi kwa huduma bora?  Huwa hatuna mawazo haya zaidi ya kutaka kupinduana kisiasa tu kila siku?  Nina hakika kama tuna hasira na maendeleo basi tunaweza tengeneza ajira za vijana walio wengi tena watoto wetu wenyewe na sio wageni ambao watakuja kuchukua hadi senti ya mwisho,  sikatai kuna sehemu lazima wataalamu wan je waingie lakini waingie kwa mkataba ambao utatutengenezea watanzania wataalamu kama ao katika vyuo vikuu vya duniani huko ambavyo vitawaamini wasomi wetu.
Kuna huduma nyingi za anga, kama kusafirisha abiria, kusafirisha mizigo, kusafirisha wagonjwa, kuzima moto, kuchukua picha, huduma za kilimo, huduma za hali ya hewa na mambo mengine ambayo yanawezekana.
Kila mara huwa naongelea suala la kujiunga na kutengeneza kitu kikubwa chenye maana kwa wananchi hiki kitu kama kweli tutafunga macho na kweli kuamua kuwekeza tunaweza kufanya jambo kubwa sana katika nchi hii,  Shirika letu litatakiwa kuwa na kiwango kisichopungua dola za kimarekani zaidi ya 10 trilioni ili kuweza kuanza angalau kwa ndege chache ndogo na kubwa.

Najua mdau unayesoma hapa una maswali mengi kuhusu jambo hili lakini kama tutakaa na kujadili na wataalamu wakaanza kuandaa Business Plan na tukafanikiwa kuanza kuchanga na mambo mengine ninaamini hili shirika linaweza kuanza na kila mmoja wetu akaja kujisifia sana huko mbele ya safari.  Tutatakiwa kujua, faida, hasara kwa upande wa fedha, usafirishaji, abiria au wateja kwa kuingia katika biashara sio kwa kulikatalia kichwani.

Siku zote ukijipa majukumu mazito utafanikiwa, lakini ukiyaachia majukumu kwa wengine huwezi kuendelea kwa kuwa maendeleo yanakutegemea wewe ili yaendelee.  Kumbuka wenye mawazo si lazima wawe wasomi, na watendaji si lazima wawe wenye fedha, bali kila mmoja anamtegemea mwenzake kwa jambo moja ama lingine.  Tushirikiane ili tuijenge Tanzania yenye mafanikio na si malalamiko


Hivi naeleweka?

Wednesday, 5 February 2014

NI MUHIMU WAZEE WATAALAM AMBAO WAMESTAAFU WATUMIKE KUJENGA TAIFA.



Ndugu mdau,
Habari yako, leo nakuja na mada hii ya wataalamu wa fani mbalimbali ambao wamestaafu muda mrefu.
Tanzania imebahatika kuwa na wataalamu wengi ambao wamepita katika Nyanja nyingi katika ajira serikalini hata katika mashirika, taasisi, wakala mbalimbali.  Wapo ambao walikuwa wanaaminika sana kwa uchapaji wao wa kazi, mawazo yao, muda mrefu wa kufanya kazi, uelewa na utambuzi wao ulioifanya Tanzania kuwa juu katika nyanja mbali mbali.
USHAURI WANGU
Haiwezekani kuanzishwa taasisi fulani ambayo itakuwa imesheheni wataalamu hao na kuwapa heshima ya kuwa wanafanya kazi kwa mkataba ili kuwapa motisha ili wasiumie katika kufuatilia mafao yao na pia utaalamu walio nao usife kabisa?  Na wale wengine basi hata wakianzisha miradi yao ya ukulima au ufugaji au hata ujenzi wa nyumba zao za kupangisha basi wapewe heshima ya miradi yao ili waweze kujipatia kipato!
Ninawaona wazee wengi wakiwa wamevaa ndala ndefu zilizowazidi miguuni mwao, wakiwa na nywele nyeupe tii, suruali zao zikiwa zimefungwa mkwiji, huku wakiwa wameshika magazeti ya zamani wakitembea huku na kule wakiwa hoi kwa njaa, na mawazo na uwezo wao wa kichwani ukiwa unatafunwa na uzee na mihangaiko wanayopata masikini, huku tukiwaangalia na kuwadharau hata wakiingia katika madaladala kwa kutowapisha katika viti, kisa hatuwajui na wamefanya makubwa sana katika nchi hii, iwe serikalini, michezoni, jeshini na sehemu nyingine.
Wengine hata wanapofuatilia mafao yao huambiwa walete CV, Barua ya ajira hivi kweli mtu alianza kazi mwaka 1970 huko leo atakuwanayo, sawa anaweza kuwa navyo vinafanyiwa kazi kwa muda? Kiinua mgongo anachopata cha miaka ya kale hakiendani hata na wakati huu kweli si tunatengeneza laana tu?
Kwanini tunawasahau wazee hawa wanakufa kihoro, wanakufa huku wakilalamika, wakisikitika, wengine wakiishi huku wakiwa wamekata tamaa  kabisa na kutoa laana kwa serikali.  Naumia sana kuona wazee hawa wakiwa hawana la kufanya zaidi ya kuwa kama wamachanganyikiwa.
Hivi hatuoni kuwa tunatengeneza nchi ya kuwahi chako haraka ili ukifikia uzee usiwe kama hawa tunaowaona kwa sasa?  Nawaomba sana jamani ambao mna shikilia sehemu ambazo zinaweza kwenda kujifunza mambo nje basi mkajifunze nchi za wenzetu wale wazee wakistaafu huwa wanatumikaje katika kuleta manufaa kwa nchi na sikuwa sahau hivi jamani.
Kwa kweli inauma sana, unakuta mtu hata ana sehemu yake ya ardhi hata iwe hekari 100, lakini anafuatilia hati miaka 30 haipati, mwisho anaonekana amehodhi ardhi bila kuitumia inavyotakiwa, mwisho linakuja wazo la kitoto kabisa eti aiachie serikali igawe kwa wengine huu ni unyama wa hali ya juu, tunatengeneza laana mbaya sana aisee, siafiki hiki kitu, na watanzania tulio wengi tunashangilia kabisa wakati yule mtu ametumikia nchi kwa miaka zaidi ya 30, na ile ndio kiinua mgongo chake, pale ndio anategemea hata awaachie wanae, ninyi hamumthamini kabisa wala kwanza hamtaki hata kuelewa, mimi nasema ni dhambi na dhambi hii itakuja kutuunguza hapa hapa duniani.
Hebu tujaribu kuvaa yale maumivu yao, machungu yao, utendaji kazi wao walioutenda kwa kujituma na uaminifu kwa miaka mingi iliyopita halafu mwisho wananyanyasika.  Inauma sana jamani.
Ndio  unatakiwa kujiandaa ili ustaafu, mzee wa watu ndio kajiandaa kanunua ardhi yake ili aje alime sasa unapomzungusha miaka nenda rudi unamaanisha unataka afe ili iweje?
Mfano mtu anastaafu na miaka 55 hadi 65 labda unamzungusha miaka 25 hadi 30 kufuatilia hati atakuwa na miaka mingapi hapo?
Najaribu tu kukumbusha wahusika, na sisi wananchi tujaribu kuliona hili lina tija.

HITIMISHO
Tujali maisha ya wengine
Tutumie wataalamu waliomaliza muda wao wa kazi na walifanya kazi kwa ueledi na kuwapa heshima kwa kuwapa taasisi moja yenye vipaji vyote humo.
Hii itachangia kuwapa motisha hata hawa waliopo madarakani wasiwaze kujilimbikizia mali pasipo sababu kwa kuwa nao wanasoma maisha ya waliopita.

Monday, 3 February 2014

JE NAWE UNATATIZO LA KUKOSA CHOO? SOMA SABABU ZA UKOSAJI CHOO NA SULUHISHO LA TATIZO HILO.

Je!Unatatizo la Kukosa Choo?

Mtu yeyote ambaye anapata walau mlo mmoja kwa siku na kupitisha kati ya siku moja au tatu bila kupata choo, ana tatizo la kukosa choo (Constipation).

NINI KINASABABISHA KUKOSA CHOO?
·         Kukosa mlo kamili.  Kama vile kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha wanga na mafuta.
·         Kula vyakula vilivyokobolewa na vilivyo changanywa na madawa ili visiharibike.
·         Mifumo hatarishi ya maisha kama vile matumizi ya sigara na pombe uliokithiri.
·         Ukosefu wa kiwango cha kutosha cha mbogamboga na matunda katika mlo, ila nakushauri ule matunda saa moja au mbili kabla ya mlo au saa moja au mbili baada ya mlo.
·         Maji yasiyo salama.
·         Kuvuta hewa chafu.
·         Na nyingine nyingi zinazosababishwa na maisha yanayoendeshwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

ATHARI ZA KUKOSA CHOO
·         Chakula kutomeng’enywa (kusagwa) vizuri.
·         Maumivu makali wakati wa kupata choo.
·         Uchafu uliokaa kwa muda mrefu kugeuka sumu.
·         Bakteria wenye madhara kuzaliwa na kuathiri utumbo mpana na viungo vingine mwilini.

NI MAGONJWA GANI SUGU YANAYOWEZA KUSABABISHWA?
·         Saratani ya utumbo mpana (colon cancer)
·         Presha
·         Kuongeza uzito (obesity)
·         Tumbo kujaa gesi
·         Magonjwa ya ini
·         Figo kushindwa kufanya kazi vizuri
·         Maginjwa ya ngozi
·         Kukakamaa kwa mishipa ya damu
·         Kisukari
·         Magonjwa ya moyo
·         Na matatizo mengine mengi

NI NINI SULUHISHO SAHIHI LA TATIZO LA KUKOSA CHOO?
Ondoa mgandamano wote wa taka katika utumbo mpana ukiuacha ikiwa msafi na wenye afya zaidi.
FAIDA YA KUONDOA MGANDAMANO
·         Ni njia haraka na salama kwa afya yako
·         Inazuia saratani ya utumbo mpana (colon cancer) na madhara mengine kiafya (coprostasis)
·         Tatizo la kukosa choo utakuwa umelimaliza
·         Utapunguza uzito uliozidi
·         Utaifanya ngozi iwe yenye afya, nyororo na muonekano mzuri

Samahani kwa kusema hivi, lakini ni ukweli uliowazi kuwa watanzania tuna aibu sana ya kuingia maliwato huku tunaangaliwa na watu wengine.  Hii ni mbaya sana kwa kuwa pale unapobana haja kubwa ukasema nitaenda baadaye unatengeneza pochi katika utumbo, chunguza mara ngapi umejibana kuanzia wakati huo hadi umri huo ulio nao, ni vipochi vingapi umetengeneza, una takataka kiasi gani katika utumbo mpana?
Utafanya mazoezi, utapunguza kula utakunywa baadhi ya dawa za kupunguza mafuta mwilini lakini utabaki na kitambi kikubwa unajua kwanini?  Kwa sababu ya vipochi ulivyovitengeneza kwa kubana choo.
Pili hata ukiingia maliwato unakimbiakimbia likitoka tonge moja basi umeshanawa umekimbia, ni hatari sana kufanya hivyo, unatakiwa ukae kuanzia dakika 10 na kuendelea ili kila kilichokuwa kinatakiwa kutoka kitoke kwa wakati huo.
Tatu, usilazimishe au usijikamue ili kutoa unachohisi kipo unachotakiwa kufanya hakikisha umejiachia na kuiacha misuli ijifungue yenyewe kwa wastani wake ili kilichopo kitoke kama kinavyotakiwa.  Ikilazimisha ndio yale yale kubakiza vipochi kila siku.
Kwa kweli wengi wetu tunakosea mambo mengi sana katika maisha yetu, kuanzia kula, kulala, kuvaa, kujisaidia haya yote ukifuatilia utakuta tunajitengenezea magonjwa bila kujua.



JE UTAJUA KUWA RANGI YA KINYESI, HARUFU YA KINYESI VINAWEZA KUKUONESHA UNA UGONJWA GANI AU BAKTERIA KIWANGO GANI?

JE UNAJUA KUWA MUUNDO AU SHAPE YA KINYESI INAWEZA KUKUTAMBULISHA UNA SHIDA GANI
·         Kama kinyesi chako ni kama ndizi uko sawa
·         Kama kinyesi chako ni kama mbuzimbuzi kuna shida aidha ya maji hunywi ya kutosha
·         Kama kinyesi kina tawanyika kama mafuta kuna shida
·         Kikiwa hakina shape pia ni shida
·         Kinyesi kikiwa kinashika katika sinki la choo ni shida kubwa sana hiyo pia
·         Kinyesi kikiwa na harufu mbaya kali ni tatizo kubwa pia

Hili ni somo nalo tutalisoma kwa kifupi naomba endelea kuingia katika blog hii kila mara kila siku

Kama utaona una matatizo au tatizo lolote katika haya niliyotaja hapa, hasa kukosa choo, vidonda vya tumbo, gesi tumboni, manyama uzembe, matatizo ya ngozi, basi wasiliana name ili tujue la kufanya.
Kwa mawazo zaidi wasiliana name nitakuelekeza cha kufanya na matatizo yako yatatuliwa.

KWA WALE WENYE MIILI MIKUBWA: HIVI NDIVYO UNAWEZA KUJUA UMEPUNGUZA UZITO WAKO KIASI GANI KWA WIKI.







MTU ANAWEZA KUPUNGUZA UZITO KIASI GANI KWA WIKI?

Mtu anaweza kupungua kilo ngapi kwa wiki ni swali ambalo watu wengi hujiuliza.Hasa pale wanapotaka kuanza harakati za kupunguza uzito. Ni wazi kwamba watu wengi hupenda kufanya Diet za muda mfupi na wapate matokea makubwa ya haraka. (umeula wa chuya, umeutengeneza huo uzito miaka mingapi unataka upungue kwa dakika ngapi?)
Kiasi cha uzito unaoweza kupunguza kwa wiki hutofautiana kati ya mtu na mtu.  Ingawa nia na juhudi binafsi huchukua nafasi kubwa katika hili, kuna mambo mengine yanayoleta tofauti hizo;
1. Jinsi
2. Umri
3. Ukubwa wa mwili
4. Vyakula unavyokula
5. Mazoezi unayofanya
Nguvu joto za chakula (kalori)
Nguvu za chakula yaani kalori, (calories) ni kiasi cha nguvu ambacho hupatikana au hutolewa na chakula kifikapo mwilini. vyakula vyote  vinaidadi fulani ya kalori isipokua maji tu ambayo hayana kalori.
Kalori hufanya kazi mwilini kama ambavyo mafuta aina ya petroli au dizeli hufanya kazi kwenye gari. Ili gari iweze kutembea lazima mafuta yaungue ili kutoa nguvu ambayo hutumika kutembeza gari,na jinsi unavyozidi kutembea ndivyo ambavyo mafuta huzidi kuungua hadi kwisha.
Mwili wa binadamu nao hufanya hivyo hivyo, nguvu unazopata kwenye chakula yaani kalori, huungua ili kutoa nguvu ambayo inauwezesha mwili wako kufanya mambo mbalimbali kuanzia kupumua, kutembea, kukimbia,na yote ambayo mwiili hufanya.  Kadiri unavyofanya shughuli nyingi zitumiazo nguvu ndivyo ambavyo kalori hupungua mwilini.
Nusu kilo ( 1/2 kg) ni sawa na kalori 3500.  Ili upunguze nusu kilo katika uzito wako nilazima utoe kalori 3500 katika mwili wako. Unaweza kutoa  kalori hizo katika mwili wako  kwa kupunguza kiasi cha kalori unazokula kwa siku au kwa kuongeza mazoezi au kufanya kazi zinazofanya utumie nguvu nyingi ili utumie nguvu za ziada ambazo mwili wako umetunza (unene wako)
Kupunguza kalori (chakula) ni muhimu zaidi kuliko kufanya mazoezi hasa kwa mtu mwenye nia ya kupunguza uzito.  Pia mtu anayepunguza uzito haraka zaidi endapo atapunguza kiasi cha kalori anazokula na kufanya mazoezi ya mwili ili kuunguza kalori ambazo mwili wake umetunza.

TOFAUTI
Jinsi ya mtu huchangia katika kuamua ni kiasi gani cha uzito anaweza kupunguza kwa wiki. Kwa kawaida wanaume wanamisuli mingi kuliko wanawake. Utafiti unaonesha kwamba misuli hutumia kalori nyingi hivyo uwepo wake katika mwili hufanya mtu aweze kupunguza uzito haraka. Hii hufanya wanaume waweze kupunguza mwili kwa haraka kuliko wanawake.
Pia tafiti hizo huonyesha kwamba mtu mwenye uzito mkubwa ana uwezo wa kupunguza uzito kwa haraka zaidi kuliko  mtu mwenye uzito mdogo, hasa mwanzoni anapoanza kupungua.
MAZOEZI

Kiasi cha kalori unachoweza kutoa mwilini unapofanya zoezi au shughuli nyingine hutokana na uzito wa mtu. Mtu mwenye uzito mdogo hutoa kalori chache na mwenye uzito mkubwa hutoa kalori nyingi kwa kiasi kilekile cha mazoezi.
Mfano:mtu mwenye kilo 72.5 atatoa calories 986 kwa kukimbia kwa dakika 60, lakini mwenye kilo 108 atatoa calories 1,472 kwa kukimbia dakika hizohizo 60
Kadiri unavyotoa  kalori nyingi mwilini ndivyo uzito unavyozidi kupungua
DIET
Diet kali hulenga kumfanya mtu apunguze uzito mwingi ndani ya muda mfupi. Tafiti huonyesha kwamba asilimia kubwa ya uzito unaopotea unapofanya diet kali ni uzito wa maji mwilini.

Ni  ngumu sana kwa mwili kutoa kilo 1 ya mafuta mwilini kwa wiki.  Hata hivyo endapo utaendelea na diet kali kwa muda mrefu basi unaweza kupunguza mafuta ya mwili na hivyo kupunguza mwili kwa haraka.
Ukifanya diet kali sana ,ambayo inakufanya uingize kalori chache sana mwilini basi kuna uwezekano wa kupunguza kilo ndani ya muda mfupi.

MAGONJWA NA MATIBABU

Historia ya afya yako ni Sababu nyingine inayochangia katika kujua kiasi cha kilo unachoweza kupunguza kwa wiki.  Magojwa yasababishwayo na homoni za mwili hufanya iwe ngumu sana kupunguza uzito wa mwili.

Tafiti zinaonyesha kwamba baadhi ya madawa kama madawa ya kisukari na dawa za uzazi wa mpango hufanya  iwe ngumu kupunguza uzito. Baadhi ya madawa pia hufanya mtu ashindwe kabisa kupunguza uzito na madawa mengine hunenepesha mwili.


USHAURI
Endapo umekua ukifanya mazoezi na diet kwa muda mrefu na hupungui uzito, ni vyema ukamuaona Daktari wako na kumuelezea hali hiyo ili aweze kutafuta chanzo cha tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi.
Kama unafanya juhudi za kupunguza uzito basi punguza kiasi cha kalori unazokula kwa siku na pia fanya mazoezi ili kuunguza kalori za akiba mwilini.
HITIMISHO.
Naamini umeelewa nikwanini hakuna kipimo maalumu cha kiasi cha uzito ambao mtu anaweza kupunguza kwa wiki, kwani vigezo vyote hivi huchangia katika kupungua.
Hata ivyo vitu kama msongo wa mawazo na kutokupata usingizi wakutosha, pia huweza kuchangia mtu kupungua uzito au kuongeza uzito.

Tukutane tena ili tupeane darasa la tiba mbadala 

Huna sababu za kutumia madawa ....